| dc.description.abstract | Utafiti huu ni wa kiisimu. Ulichunguza peo za utambulisho katika diskosi za wabunge wanawake kutoka Bunge la Taifa nchini Kenya. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza peo za utambulisho katika diskosi zilizotumiwa na wabunge wanawake kujitambulisha kwa umma. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Peo na mtazamo wa Uchanganuzi Hakiki-Makinifu wa Usemi. Nadharia ya Uchanganuzi Peo
ilisaidia kubainisha matini za mahusiano katika diskosi ili kupata muundo bora katika uundaji wa peo na katika usanisi wa mchango wa peo katika mawasiliano. Mtazamo wa Uchanganuzi Hakiki-Makinifu wa Usemi ulisaidia kupata maana ya diskosi katika muktadha wa jamii, mchango wa diskosi hiyo, mahusiano ya kiuwezo baina ya watumiaji wa diskosi na utambulisho uliojitokeza kutokana na matumizi ya diskosi husika. Chanzo cha data katika utafiti huu ni video kutoka mtandao wa YouTube zikihusu hotuba za wabunge wanawake pamoja na hotuba za mikutano yao wakihutubia umma. Mbinu ya utafiti iliyotumika kukusanya data ilikuwa utazamaji na usikilizaji. Msimbo-Matini pamoja na Mwongozo wa Usimbaji (MMMU) ulitumika kama kifaa cha kupanga matini za diskosi zilizotumika kipeo wakati wa kujitambulisha kwa wabunge wanawake kwa wananchi. Mtafiti alichunguza hotuba 69 kutoka kwa wabunge wanawake 169 waliochaguliwa na wananchi katika Bunge la Taifa la Kenya la 11, 12 na 13. Wasailiwa hao walikuwa wanawake 111 waliowakilisha kaunti pamoja na wanawake 58 waliochaguliwa kuwakilisha maeneobunge mbalimbali katika bunge la 11, 12 na 13 la taifa la Kenya. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa matumizi ya kiisimu ya leksikoni, kwenye diskosi za wabunge wanawake, hutegemea mahitaji ya kibinafsi na kivikundi na zilitambulisha wabunge wanawake katika kiwango cha kibinafsi, kieneo na kivikundi. Kupitia leksikoni hizo, peo za utambulisho zilidhihirisha migao ya kibinafsi, kimaeneo, kimahusiano, kiutendaji na kivikundi katika ujenzi wa jinsia ya kike. Vilevile, ulibaini kuwa sitiari, ulinganisho, masimulizi ya siasa na matumizi ya virainasa ni miongoni mwa mbinu za peo zilizotumika katika diskosi za wabunge wanawake katika Bunge la Taifa. Aidha, mahusiano ya kiuwezo kati ya wabunge wanawake na wapiga kura hukuzwa na peo za utambulisho ambapo wabunge wanawake wamejengwa kama wasaidizi na wakombozi wa wapiga kura. Zaidi ya hayo, panapotokea migogoro kati ya kiongozi mwanamke na wapiga kura, kiongozi mwanamke hujitambulisha na kikundi kinachoathirika. Mahusiano kati ya wabunge wanawake na wabunge wanaume yalitambulisha wanawake kama waathiriwa wa ubaguzi. Aidha, Peo za utambulisho katika diskosi za wabunge wanawake zilichangia kudumisha mamlaka, kubadilisha hali fulani za jinsia na kukarabati hali-ante kuhusiana na jinsia na mamlaka katika Bunge la Taifa la Kenya. Mwisho, utafiti huu
umependekeza tafiti zifanywe kuhusu uwezo wa lugha katika kuunda, kudumisha na kubadilisha peo ya kutambulisha jinsia ya kiume na majukumu yake katika udumishaji wa mahusiano ya mamlaka katika mazingira yanayobadilika kwenye nyanja anuwai za jamii. Utafiti zaidi unaweza kufanywa ili kutathmini nia na sababu za wabunge wanawake kupendelea kujitambulisha kama mama wala si mwakilishi wa kaunti ama
mbunge wanapotambulisha nafasi zao katika diskosi za siasa. Hatimaye, ni muhimu utafiti zaidi ufanywe kuhusu miundo na maumbo ya maneno yanayotumiwa na wabunge wanawake katika diskosi zao ili kuunda mahusiano ya mamlaka. | en_US |